Cyril Ramaphosa
Matamela Cyril Ramaphosa (alizaliwa 17 Novemba 1952) ni mwanasiasa kutoka nchini Afrika Kusini aliyeapishwa kama rais wa nchi tarehe 15 Februari 2018. Aliwahi kuwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Afrika Kusini, mpiganiauhuru na mfanyabiashara anayehesabiwa kati wa matajiri wa nchi yake. Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa Makamu wa rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini. Mnamo Desemba 2017 alichaguliwa mwenyekiti wa chama cha African National Congress (ANC). Maisha ya awali na elimuMatamela Cyril Ramaphosa alizaliwa huko Johannesburg[1]. Alikuwa mtoto wa pili kati ya watatu wa Erdmuth na Samuel Ramaphosa aliyekuwa afisa wa polisi. Alikulia katika eneo la Soweto aliposoma shule ya msingi na ya sekondari akamaliza shule mwaka 1971. Mwaka 1972 alianza masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Kaskazini (Turfloop) kilichokuwa chuo kwa ajili ya Wasotho, Wavenda na Watsonga katika mfumo wa apartheid. Huko chuoni Ramaphosa alianza kushiriki katika siasa ya wanafunzi na vyama kama South African Students Organisation (SASO) na Mkongamano wa Watu Weusi (BPC). Hivyo alikamatwa na serikali ya apartheid na kufungwa jela miezi 11 kwa mashtaka ya kusaidia ugaidi. Alirudishwa jela mwaka 1976 baada ya ghasia za Soweto[2]. Baada ya kutoka kizuizini akawa karani katika kampuni ya wanasheria mjini Johannesburg akiendelea na masomo yake kwa njia ya barua. Mwaka 1981 alipokea shahada ya sheria. Mwanaharakati wa kisiasa na kiongozi wa chama cha wafanyakaziMwaka uleule aliajiriwa kuwa mshauri wa sheria katika ofisi ya kimoja kati ya vyama mbalimbali vya wafanyakazi (National Council of Trade Unions NCTU). Mwaka 1982 alipewa jukumu la kuunda chama kipya cha National Union of Mineworkers (NUM) kama kitengo cha NCTU. Ramaphosa alikamatwa tena katika bantustan ya Lebowa kwa kuhudhuria mkutano uliopigwa marufuku[3]. Hata hivyo alifaulu kuunda chama hicho akachaguliwa kuwa katibu wake. Mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangiAkiwa kiongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi (NUM) Ramaphosa aliandaa mikutano ya harakati mbalimbali kati ya wafanyakazi wa Afrika Kusini kwa shabaha ya kuiunganisha. Ramaphosa alikuwa mwenyekiti wa mkutano wa Soweto mnamo Juni 1985 ambako wawakilishi wa vyama mbalimbali walipatana kuunda shirikisho la kitaifa kwenye msingi wa kutojali rangi na kuwa na chama kimoja kwa kila tasnia[4]. Mkutano wa Desemba 1985 uliohotubiwa na Ramaphosa ulileta maungano ya Congress of South African Trade Unions (COSATU). Ramaphosa alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa maungano mapya. Chini ya uongozi wake, uanachama uliongezeka kutoka 6,000 mwaka 1982 hadi 300,000 katika 1992. Karibu nusu ya wafanyakazi Waafrika wote katika migodi walikuwa wanachama. Akiwa katibu mkuu aliongoza mgomo mkubwa katika migodi katika historia ya Afrika Kusini. Mwaka 1986 Ramaphosa aliongoza kamati ya COSATU iliyosafiri Zambia kwa kukutana na ANC. Katika miaka iliyofuata alizuiliwa kwa muda kurudi Afrika Kusini. Mwaka 1990 serikali ya rais Frederik Willem de Klerk ilifuta sheria iliyopiga ANC marufuku. Ramaphosa aliingia katika kamati ya kumpokea Nelson Mandela aliyetakiwa kuondoka gerezani na kufanya ziara katika nchi. Mwezi Julai 1991 Cyril Ramaphosa alichaguliwa Katibu Mkuu wa ANC na baada ya uchaguzi alijiuzulu katika nafasi yake kwenye chama cha wafanyakazi COSATU. MwanasiasaMwaka 1991 aliteuliwa kuongoza kamati ya African National Congress iliyokutana na wawakilishi wa serikali ya De Klerk ili kutafuta mapatano jinsi ya kumaliza apartheid[5]. Katika uchaguzi huru wa kwanza wa mwaka 1994 alichaguliwa kuwa mbunge akawa mwenyekiti wa bunge la katiba lililokutama mwaka 1994 kuunda katiba mpya ya Afrika Kusini[6]. Mfanya biasharaMwaka 1997 alishindwa na Thabo Mbeki kupata nafasi ya makamu wa rais wa nchi akajiuzulu katika vyeo vyote vya kisiasa[7]. Hapo aliingia katika maisha ya uchumi akishika nafasi mbalimbali katika makampuni makubwa pamoja na kuunda kampuni ya New Afrika Investments Ltd. Hata hivyo alichaguliwa kuingia katika Halmashauri Kuu ya ANC akarudishwa mwaka 2007. Ramaphosa alifaulu katika shughuli za biashara akihesabiwa kuwa mmoja wa matajiri wa Afrika Kusini[8]. Makamu wa raisMwaka 2012 Ramaphosa aligombea nafasi ya makamu wa mwenyekiti wa ANC akachaguliwa[9] akaendelea kuwa makamu wa rais Jacob Zuma. Mwenyekiti wa ANC na rais wa Afrika KusiniKatika mkutano mkuu wa ANC wa Desemba 2017 Ramaphosa alimshinda Nkosazana Dlamini-Zuma (mke wa zamani wa rais Zuma) akawa mwenyekiti wa ANC. Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa alitangaza nia yake ya kumaliza rushwa katika taifa [10]. Mwezi Februari 2018 Kamati Kuu ya ANC chini ya uongozi wa Ramaphosa ilidai Rais Zuma ajiuzulu. Baada ya Zuma kukataa awali, kundi la wabunge wa ANC ilitangaza nia ya kumwondoa rais madarakani, hivyo Zuma akajiuzulu. Tarehe 15 Februari Ramaphosa akachaguliwa na bunge kuwa rais mpya wa Afrika Kusini.[11][12] Mnamo Februari 10, 2020, Cyril Ramaphosa anapaswa kuchukua urais wa Jumuiya ya Afrika, akifaulu na Abdel Fattah al-Sissi. Marejeo
Viungo vya nje
|