Share to: share facebook share twitter share wa share telegram print page

 

Makaburu

Jan van Riebeeck na wenzake wakifika Afrika Kusini, mchoro wa Charles Bell.

Makaburu (kutoka Kiholanzi na Kiafrikaans boer inayomaanisha mkulima) ni jina la walowezi Wazungu wa Afrika Kusini na Namibia wanaotumia lugha ya Kiafrikaans. Wenyewe wanajiita mara nyingi Afrikaner yaani "Waafrika".

Wako takriban theluthi mbili ya Wazungu wa Afrika Kusini au milioni 1.5. Karibu wote ni Wakristo Waprotestanti hasa wa madhehebu ya Kikalvini.

Baada ya kushindwa katika vita vya pili vya Makaburu dhidi ya Uingereza mwaka 1902, tena baada ya mwisho wa siasa ya apartheid, vikundi vya Makaburu walihamia nje ya nchi kwenda nchi nyingine za Afrika na pia za Amerika.

Historia

Mababu wao ni mchanganyiko wa wahamiaji kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani, waliofika tangu mwaka 1652 katika koloni la Kampuni ya Kiholanzi ya India ya Mashariki. Walikaa huko kama wakulima waliouza mazao kwa meli zilizozunguka kati ya Uholanzi na makoloni ya kampuni katika Indonesia ya leo.

Mwaka 1814 ambapo Uingereza ilitwaa utawala juu ya Koloni ya Rasi na hapo sehemu ya Makaburu walianza kuondoka katika eneo la koloni na kuingia katika nchi upande wa kaskazini walipounda jamhuri zao kama Transvaal, Dola Huru la Oranje na Natalia.

Hasa kufutwa kwa utumwa mwaka 1834, sheria ya kufanya Kiingereza lugha rasmi na matumizi ya sheria za Uingereza vilisababisha kuondoka kwa Makaburu wengi katika koloni ya Rasi waliojulikana kama Voortrekker.

Jamhuri za Makaburu zilitwaliwa polepole na Waingereza waliowafuata walikohamia. Jamhuri ya Transvaal ilitambuliwa na Uingereza mara ya kwanza mwaka 1852; ilitwaliwa mwaka 1877 lakini baada ya vita vya kwanza vya Makaburu dhidi ya Uingereza uhuru wake ulitambuliwa tena.

Waziri mkuu wa serikali ya koloni ya Rasi Cecil Rhodes alikuwa adui wa uhuru wa Makaburu na baada ya kupatikana kwa almasi katika eneo la Johannesburg alijaribu kupindua serikali ya Transvaal. Hii ilisababisha vita vya pili vya Makaburu dhidi ya Uingereza. Waingereza walishinda na katika amani ya Vereeniging Makaburu walipaswa kukubali ubwana wa Uingereza. Lakini miaka kadhaa baadaye Uingereza uliwapa Makaburu haki ya kujitawala katika mambo ya ndani.

Mwaka 1910 maeneo ya Kiingereza pamoja na majimbo ya Makaburu yaliungana kuwa Muungano wa Afrika Kusini. Hapo lugha ya Kiholanzi (lugha mama ya Kiafrikaans) ilitambuliwa kama lugha rasmi ya nchi pamoja na Kiingereza. Mwaka 1925 Kiafrikaans ilikubaliwa kama lugha rasmi badala ya Kiholanzi.

Chama cha kisiasa kilichopigania haki na matakwa ya Makaburu kilikuwa hasa chama cha National Party (Afr.: Nasionale Party). Mwaka 1948 chama hiki kilipata kura nyingi kikaanzisha siasa ya Apartheid iliyodumu hadi mwaka 1990.

Makaburu wengi waliendelea kupigia kura National Party na hivyo kudumisha siasa ya ubaguzi wa rangi hadi mwisho wake 1990, ambapo viongozi walikubali ya kwamba haiwezekani kusimamia nchi dhidi ya mapenzi ya wananchi wengi yaani Waafrika waliobaguliwa katika muundo wa Apartheid.

Tazama pia

Marejeo

Viungo vya nje

Prefix: a b c d e f g h i j k l m n o p q r s t u v w x y z 0 1 2 3 4 5 6 7 8 9

Portal di Ensiklopedia Dunia

Kembali kehalaman sebelumnya