Mlipuko mkuuMlipuko mkuu au mlipuko asilia (kwa Kiingereza Big Bang) ni nadharia ya kisayansi kuhusu chanzo cha ulimwengu inayojaribu kueleza sababu ya kutokea kwa nyota, magalaksi na anga kwa jumla jinsi tunavyoviona leo. Kutokea kwa ulimwenguKufuatana na nadharia hii ulimwengu ulitokea mahali pamoja padogo sana penye joto na densiti kubwa, pasipo na nyota wala atomi wala umbo lolote. Hali hiyo inaelezwa ilikuwa ya pekee. Takriban miaka bilioni 14 iliyopita [1] anga ya ulimwengu lilianza kupanuka haraka na katika mchakato huo atomi ziliundwa zilizoendelea kujenga mata tunavyoijua na kuwa nyota na magalaksi. Ulimwengu unaendelea bado kupanuka na wakati huohuo kupoa. Nafasi ya ulimwengu inapanuka na katika mwendo huu halijoto inapungua. JinaJina la "Big Bang" lilibuniwa na mwanafizikia Fred Hoyle aliyepinga nadharia hii, lakini wengine walioitetea walipenda jina, hivyo likabaki. [2] Athari ya Doppler na mlipuko mkuuSababu za kubuni nadharia ya mlipuko mkubwa ni kutafuta maelezo kwa vipimo vinavyopatikana kuhusu anga ya ulimwengu. Sababu muhimu zaidi ni mabadiliko ya nuru ya galaksi ambazo zinaonekana kuwa mbali sana. Nuru hiyo inasogea kwa upande wa nyekundu zaidi katika spektra yake. Huu msogeo wekundu (ing. redshift) wa nuru ya nyota za mbali huelezwa kwa athari ya Doppler. Maana yake ni kwamba, kama kitu kinaelekea kwenda mbali nasi, rangi yake huelekea kuwa nyekundu zaidi kwa sababu mwendo wake hupanusha masafa ya mawimbi ya nuru. Nyekundu ina urefu mkubwa zaidi kati ya mawimbi ya nuru ya rangi zinazoonekana. Kadiri jinsi mwelekeo mwekundu unavyoongezeka vile, kitu kina mwendo wa haraka zaidi kuelekea mbali nasi. Dalili nyingine ni mnururisho wa mandharinyuma (ing. cosmic background radiation) uliowahi kutabiriwa kinadharia na wanafizikia tangu miaka ya 1930. Iligunduliwa na kuthibitishwa kwa njia ya vipimo tangu mwaka 1964. Huu ni mnururisho dhaifu sana usio na asili katika nyota au galaksi yoyote; leo hii wanasayansi wengi wanaiona kama mabaki ya nishati wa mlipuko mkuu inayoendelea kijaza ulimwengu. Kutokana na vipimo hivyo wanasayansi wengi kabisa wa fizikia na astronomia wanaona ya kuwa nadharia ya mlipuko asilia inaeleza vizuri zaidi vipimo vinavyopatikana kuhusu ulimwengu. [3] Nadharia hii inaonekana pa kupatana na makadirio kuhusu viwango vya elementi vya kikemia vinavyogunduliwa katika anga ya ulimwengu. Kuna tofauti ya mawazo kama mlipuko mkuu ulikuwa chanzo kabisa cha ulimwengu au kama uliwengu mwingine ulikuwepo kabla yake, na labda mwendo wa kupanuka unaweza kurudishwa katika mwendo wa kukaza siku moja hadi mata yote kuwa mahali pamoja na kulipuka tena. [3] Falsafa na diniNadharia hii ina umuhimu pia kwa falsafa na dini, ambazo pia zinaeleza chanzo cha ulimwengu, k.mf. kwa kusema umeumbwa na Mungu. Kuna wafuasi wa dini mbalimbali wanaopinga nadharia hiyo wakiona hailingani na imani yao. Kinyume chake wako wengine wanaosema kuwa nadharia ya mlipuko mkubwa inalingana vema na hoja ya uumbaji unaoendelea kupitia sheria za maumbile zinazozidi kugunduliwa na sayansi. Mwanzilishi mwenyewe wa nadharia hiyo alikuwa Georges Lemaitre (1894-1966), padre wa Kanisa Katoliki kutoka Ubelgiji. Ndiye aliyependekeza nadharia hiyo mwaka 1927, akifuatwa na wengine wengi zaidi na zaidi. Kwa mtazamo wa padri huyo na Wakristo wengine kadhaa ni kwamba si lazima kusadiki masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji yanaeleza matukio kihistoria au kisayansi, bali yanadai msomaji akubali kuwa asili ya vitu vyote vilivyopo ni Muumba. Tazama piaTanbihi
Marejeo
|