Chlodvig IChlodvig I (tamka Klod-vig; jina linaandikwa pia kwa namna mbalimbali Chlodowech au Clovis, baadaye lilikuwa Kifaransa Louis na Ludwig wa Kijerumani wa kisasa; 466 hivi - 27 Novemba 511) alikuwa mfalme wa kwanza wa Wafaranki aliyeunganisha sehemu kubwa ya taifa hilo. Alimrithi baba yake Childeric I mwaka 481 [1] kama mfalme wa Wafaranki katika eneo la magharibi mwa Rhine ya chini wakati huo. Kitovu chao kilikuwa karibu na Tournai na Cambrai kwenye mpaka wa kisasa kati ya Ufaransa na Ubelgiji [2]. Clovis alishinda makabila jirani ya Wafaranki akajiimarisha kama mfalme pekee kabla ya kifo chake. Chlodvig aliongokea Ukatoliki, kinyume na Ukristo wa Kiario ambao ulikuwa wa kawaida miongoni mwa makabila ya Wagermanik. Baada ya kumwoa Klotilde wa Burgundia aliyekuwa Mkatoliki, Chlodvig alibatizwa katika Kanisa Kuu la Reims. Hatua hiyo ilikuwa muhimu sana katika historia ifuatayo ya Ufaransa na Ulaya Magharibi kwa ujumla. Mfalme Mkristo Mkatoliki alipunguza tofauti kati ya wananchi wa Gallia waliokuwa Wakatoliki na watawala wapya Wafaranki ambao wengi walikuwa Wapagani au Wakristo Waario. Hatua hiyo iliongeza nguvu yake ikamwezesha kupanua utawala wake karibu na jimbo lote la kale la Kirumi la Gallia (takriban Ufaransa ya kisasa). Chlodvig anatazamwa kuwa mwanzilishi wa Ufaransa na nasaba ya Wamerovingi, ambayo ilitawala Wafaranki kwa karne mbili zilizofuata. Marejeo
VyanzoWikimedia Commons ina media kuhusu:
|