WagermanikWagermanik (kutoka Kilatini "Germani" kupitia Kiingereza "Germanic people") ni jina la kundi la kihistoria la makabila na mataifa yenye asili ya Ulaya Kaskazini ambayo hujumuishwa kutokana na lugha zao zilizofanana. Lugha hizo zinazoitwa lugha za Kigermanik ni kundi ndani ya lugha za Kihindi-Kiulaya. Lugha za Kigermanik huzungumzwa leo hii na wasemaji wa Kijerumani, Kiingereza, Kiholanzi, Afrikaans, lugha za Skandinavia na nyinginezo, lakini kwa kawaida wasemaji wa leo hawaitwi tena "Wagermanik" bali huangaliwa kama ukoo wa baadaye wa Wagermanik wa kale. JinaJina la Wagermanik lilitokea mara ya kwanza kutoka kwa waandishi wa Roma ya Kale. Julius Caesar aliandika juu ya makabila waliokaa upande wa mashariki wa Wakelti wa Gallia kwa kuwataja kama "Germani" na watu waliokalia nchi ya "Germania". Hata Caesar hakujua mengi sana juu yao: aliwatambua tu kama tofauti na Wakelti wa Gallia. Hadi leo haijulikani kama kiasili walijiita hivyo wenyewe au kama ni zaidi majirani waliowaita "Germani". Nadharia ya zamani ilisema hao "Germani" walijiita wanaume au watu (="man, mani") wenye mikuki ("ger"). Lakini siku hizi wataalamu wengi zaidi wanaona ya kwamba ni Wakelti waliowaita ama "majirani" au "watu wa msituni" kwa neno fulani la Kikelti. Wagermanik, Udachi, Wajerumani, Germans, Germany, Teutonic, GermaniaKatika Kiswahili cha leo maneno "Ujerumani" na "Wajerumani" humaanisha nchi kubwa ya kisasa katika Ulaya ya Kati na wakazi wake. Majina haya yametokana na kawaida ya lugha ya Kiingereza kuita nchi hiyo "Germany" na wenyeji wake "Germans". Katika hilo lugha ya Kiingereza inafuata kawaida ya Kilatini kilichoita nchi iliyopo upande wa mashariki wa Gallia kwa jina la "Germania" na wakazi wake "Germani". Lakini wenyeji wenyewe leo hii wanajiita "Deutsch" (tamka: doitsh) na nchi yao "Deutschland" (tamka: doitshland). Hii inalingana na neno jingine la Kiswahili "Udachi / Wadachi" lililokuwa kawaida kabla ya ukoloni wa Kiingereza. Lakini neno la Kilatini "Germani" lilitaja watu wengi zaidi kuliko wakazi wa Ujerumani = Germany = Deutschland wa leo. Liliendelea kumaanisha pia wengine waliozungumza lugha za Kigermanik waliokaa Ulaya ya Kaskazini na Ulaya ya Mashariki na kushiriki katika uhamisho mkuu wa Ulaya wakati wa karne ya 4 hadi ya 8 na kufikia hadi Afrika ya Kaskazini. Kwa Kiingereza jumla ya makabila au mataifa hayo liliitwa pia kwa jina la "Teutonic peoples / Teutonic tribes" kutokana na kabila lililojulikana kwa Waroma wa Kale kama Teutoni. Asili ya WagermanikAsili ya Wagermanik haijulikani kikamilifu. Inaaminiwa leo ya kwamba wasemaji wa lugha asilia ya Kigermanik walikaa mwanzoni katika Skandinavia na Ujerumani ya Kaskazini hadi takriban mwaka 750 KK. Wakati ule kuna uwezekano wa kwamba kipindi cha hali ya hewa baridi kilisababisha njaa katika maeneo yao na kuwafanya wahamie kusini wakifuata pwani za bahari na mabonde ya mito mikubwa kama Rhine, Elbe, Oder na Vistula. Caesar aliwakuta kando ya mto Rhine mnamo mwaka 50 KK. Mwandishi Mroma Tacitus aliwajua wengine waliokaa kaskazini na mashariki zaidi. Waroma waliandika ya kwamba walipenda vita, walikuwa na wafalme waliochaguliwa katika mkutano wa wanaume huru waliovaa silaha, walikula nyama ya kuchoma na kunywa bia au divai. Waroma walijaribu kupanua utawala wao ndani ya Germania lakini baada ya kushindwa na Wagermanik mnamo mwaka 9 BK walijenga maboma mengi na ukuta mkubwa kando ya mito Rhine na Danubi kama mpaka wa kudumu dhidi yao. Uhamisho mkuu wa UlayaWagermanik walihama mara kadhaa kwa karne nyingi. Majaribio ya makabila ya Kigermanik kuingia Italia yalirudishwa na jeshi la Roma katika karne ya 2 KK. Katika karne ya 2 BK kabila la Wagothi lilianza kuhamia kusini kutoka bonde la Vistula kuelekea Bahari Nyeusi. Huko waligongana na Wagermanik wengine na kuwasababisha kuingia katika eneo la Kiroma kwenye Balkani. Miendo hiyo bado ilihusika vikundi visiyokuwa vikubwa sana na Dola la Roma liliweza kuwapokea watu wa makabila hayo na kuwatumia kama wanajeshi au kama walowezi waliokubali ubwana wa Kiroma ndani ya mipaka ya dola. Lakini katika karne ya 4 makundi makubwa ya watu walielekea Ulaya kutoka Asia ya Kati: hao walikuwa makabila ya Wahunni. Walienea kwa nguvu wakasababisha uhamisho mkubwa kati ya Wagermanik walioendelea kuhamia upande wa kusini na magharibi. Kuanzia karne ya 4 hadi mwaka 700 makabila mengi ya Wagermanik walihamahama katika Ulaya ama kwa sababu walishambuliwa na Wahunni au Wagermanik wengine au kwa sababu waliona nafasi ya kuingia katika maeneo tajiri zaidi ya majirani waliodhoofishwa na vita kutokana na harakati hiyo ya uhamisho mkuu. Dola la Roma lilishindwa kujihami dhidi ya watu wengi hao waliofika kwenye mipaka yake, likaanza kuwaruhusu kuingia ndani ya eneo lake na kuwapa ardhi ya kulima na kujenga makazi. Kadiri uwezo wa Roma ulivyopungua makabila ya Wagermanik waliowahi kuingia walianza kuasi dhidi ya mamlaka ya Kiroma na kuhama tena. Katika miaka 150 ya kwanza ya uhamisho mkuu uwezo wa Dola la Roma uliporomoka kabisa na mwaka 476 wanajeshi wa Kigermanik katika jeshi la Kiroma walimpindua Kaisari na kuchukua utawala katika Italia. Makabila mengine yalianzisha falme zao katika Italia, Hispania na pia Afrika ya Kaskazini kama Wavandali. Falme za makabila hayo yalikuwa kiini cha mataifa ya kisasa katika nchi kadhaa lakini penginepo madola ya Wagermanik yalipotea kabisa. Kati ya falme muhimu za Kigermanik ni hasa ule wa Wafaranki walioanzisha milki yao katika maeneo ya Ufaransa na Ujerumani ya leo ambazo zilikuwa chanzo cha nchi za kisasa.
|