WahunniKuhusu watu wakorofi wasio na maadili mema, angalia Wahuni Wahunni walikuwa watu wa makabila mbalimbali kutoka Asia ya Kati walioanza kuelekea magharibi wakati wa karne ya 4 na ya 5 BK na kuvamia Ulaya, Uajemi na Uhindi. Chanzo katika Asia ya KatiKiasili walitokea katika maeneo kati ya Kirgizia na Mongolia ya leo. Hakuna uhakika kuhusu utamaduni na lugha yao. Wataalamu wengi walifikiri kuwa walikuwa mchanganyiko wa makabila mbalimbali kati yao Waturuki na pia Wamongolia. Siku hizi inaonekana sehemu kubwa walikuwa makabila ya Kiirani. Kwa jumla walikuwa wahamiaji waliofuga farasi na wanyama wengine na kuishi katika hema kwa muda mwingi. Sababu ya kuhama kwao haijulikani. Kuna taarifa ya kwamba wahamiaji wa Asia ya kati walishindwa na Wachina mnamo mwaka 352. Kwa hiyo inawezekana kwamba makabila yalianza kuelekea magharibi baada ya kushindwa hivyo. Wengine husema palikuwa na mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoongeza ugumu wa maisha na kuwasababisha kutafuta nchi mpya. Kufika UlayaKuanzia mwaka 374 Wahunni walifika katika maeneo ya mto Volga na kushambulia makabila ya Kigermanik waliokaa kule. Wakaendelea kuhamia magharibi na kuvamia nchi nyingi. Waliogopwa sana kwa sababu ya ukatili wao na mbinu zao za kushambulia haraka. Hawakuwa na wanajeshi wa miguu bali walipanda farasi na kutumia hasa pinde na mishale. Kwa njia hiyo wakasababisha mwendo mkubwa unaoitwa "uhamisho wa mataifa" katika historia ya Ulaya kati ya karne ya 5 na karne ya 6. Wahunni kama chanzo cha uhamisho wa mataifa katika UlayaMashambulio ya Wahunni yalisababisha makabila mengi ya Wagermanik kukimbia wakielekea magharibi vilevile na kuingia katika maeneo ya Dola la Roma. Uvamizi huu wa Wagermanik waliokuwa wakimbizi mbele ya Wahunni ulidhoofisha Dola la Roma na kuwa sababu kuu ya mwisho wake. Kati ya Wagermanik waliokimbia walikuwepo pia Wavandali walioendelea kuhamahama hadi Afrika ya Kaskazini. Attila kuongoza Wahunni woteWahunni walikuwa na udhaifu bado kwa sababu waligawanyika katika vikundi vingi. Mnamo mwaka 433 Attila alifaulu kushika utawala wote peke yake. Aliwakusanya Wahunni wengi kwenye makambi makubwa katika eneo la Panonia (Hungaria ya leo). Kutoka huko walishambulia nchi jirani; hawakuwa na kusudi la kuteka nchi hizo bali kupora nchi, kuiba mifugo na vyakula na kudai pesa ili wasiendelee. Attila aliharibu miji na vijiji vya nchi za Balkani na kuingia hadi Germania (Ujerumani), Gallia (Ufaransa) na Italia, ambapo alirudishwa nyuma na Papa Leo I. Mwaka 451 alishindwa na mabaki ya jeshi la Roma pamoja na makabila ya Kigermanik katika eneo la Ufaransa ya magharibi. MwishoBaada ya kifo cha Attila watoto wake walishindana kuhusu urithi. Mmojammoja walishindwa sasa na Roma ya Mashariki na Wagermanik. Wahunni walitawanyika na kupotea katika historia. Mabaki yao yalimezwa na makabila mengine.
|