Gregori wa NarekGregori wa Narek (kwa Kiarmenia Գրիգոր Նարեկացի, Grigor Narekatsi; 951 hivi - 1003 hivi) alikuwa mmonaki na padri wa Armenia maarufu kama mwanafalsafa, mwanateolojia na mtakatifu wa Kanisa la Kitume la Armenia. Mzaliwa wa familia ya washairi, akiishi katika monasteri ya Narek (Narekavank), ni "mshairi mkuu wa kwanza wa Armenia".[1] "Kitabu cha Sala", ambacho pengine kinajulikana kama "Kitabu cha Maombolezo", ni kati ya maandishi bora ya fasihi ya Kiarmenia na kimetafsiriwa katika lugha nyingi. Papa Fransisko alimtangaza mwalimu wa Kanisa tarehe 12 Aprili 2015. MaishaGregori alizaliwa Andzevatsik mwaka 950 hivi katika familia ya wakleri wasomi. Baba yake, Khosrov Mkuu, kisha kufiwa mapema mke wake, alipata kuwa askofu mkuu akaandika vitabu muhimu vya teolojia. Mama alipofariki, Gregori alikabidhiwa alelewe na jamaa yake, Anania wa Narek, mwanzilishi wa monasteri na shule ya kijiji hicho. Tangu utotoni hadi kifo chake, Gregori aliishi katika monasteri hiyo maarufu kama Narekavank, kwenye Ziwa Van, huko Vaspurakan, Ufalme wa Armenia, leo nchini Uturuki. Milenia ya kwanza ya Ukristo ilipokaribia kutimia, monasteri ya Narek ilikuwa kitovu maarufu cha elimu kwa Waarmenia. Ikikuwa miaka ya utulivu kabla ya uvamizi wa Waturuki na Wamongolia uliobadili moja kwa moja historia ya Armenia. Miaka hiyo Armenia ilikuwa inapitia kipindi cha ustawi wa mpya wa fasihi, uchoraji, usanifu majengo na teolojia, ambao ulichangiwa sana na Mt. Gregori, mwalimu wa shule ya monasteri. Monasteri hiyo ilibomolewa kabisa katika karne ya 20, baada ya Maangamizi ya Waarmenia yaliyofanywa na Waturuki kuanzia mwaka 1915. Utafiti uliofanywa hivi karibuni kuhusu maandishi yake unadokeza kwamba alifahamu vitabu vya Ugiriki wa kale vilivyotafsiriwa katika Kiarmenia. Kwa mfano, kwamba alijua sana vile vya Plato, Aristotle, Porfiri, Plotino na Filo wa Aleksandria. Hiyo ilichangia kumfanya ashukiwe kama baba yake kuwa mzushi, yaani kufuata mafundisho ya Mtaguso wa Kalsedonia tofauti na waliofanya Waarmenia wengi. Kitabu cha SalaKitabu hicho kimejulikana kwa muda mrefu kama kimojawapo kati ya vile bora vya Ukristo wote. Gregori alikiita "kamusi elezo ya sala kwa mataifa yote" kwa sababu alitumaini kitaongoza watu wa dunia nzima katika sala. Akiombwa na wanajumuia wenzake, alilenga kupata jibu kwa swali gumu: "Mtu anaweza kumtolea nini Mungu, muumba wetu, ambaye anavyo tayari vitu vyote na anajua yote vizuri kuliko tunavyoweza kuyaeleza sisi?" Swali hilo walilojiuliza manabii, watunzi wa Zaburi, mitume na watakatifu, alilijibu kwa unyenyekevu – kama mlio wa moyoni. Katika sala 95, Gregori alitumia uwezo wote wa lugha ya Kiarmenia ili kutafsiri hisia za uchungu na unyenyekevu katika toleo la maneno yaliyofikiriwa kumpendeza Mungu. Alikiita wasia wake: "herufi zake kama mwili wangu, ujumbe wake kama roho yangu"; ni jengo la imani kwa nyakati zote, la pekee katika fasihi ya Kikristo kutokana na mifano yake yenye ubunifu mwingi, teolojia yake ya dhati, ujuzi wake wa Biblia na unyofu wa mawasiliano yake na Mungu. Mwaka wa uandishi haujulikani vizuri, lakini ulimalizika miaka 1001-1002, mwaka mmoja kabla hajafa. Kwake ni lazima lengo kuu la binadamu wote liwe kumfikia Mungu, na kutumia yale yote ambayo umbile linawapatia ili kuungana naye, kwa kufuta tofauti zilizopo kati yao na yeye. Muungano huo unawezekana si kwa njia ya mantiki bali ya hisia. Hapo matatizo ya maisha haya yangekoma. Maandishi mengineGregori alifafanua kifumbo Wimbo Ulio Bora (mwaka 977, ambapo alipata upadirisho) na kuandika vitabu vingi vya mashairi, sala na hotuba, mbali ya Historia ya msalaba wa Aparan na kitabu kimoja dhidi ya Watondrakiti (Wapauliciani). Heshima katika Kanisa KatolikiGregori ya Narek anaheshimiwa kama mtakatifu na Waorthodoksi wa Mashariki, Kanisa Katoliki la Armenia na Kanisa Katoliki lote, jina lake likiwemo katika orodha rasmi kwenye tarehe 27 Februari[2]. Papa Yohane Paulo II alimtaja katika hotuba mbalimbali[3][4][5] na katika hati Redemptoris Mater[6] na katika barua kwa ajili ya miaka 1,700 ya Ubatizo wa Taifa la Armenia.[7] Tena anatajwa katika namba 2678 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki.[8] Tarehe 21 Februari 2015, Papa Fransisko alitangaza nia yake ya kumfanya mwalimu wa Kanisa,[9][10][11] akatekeleza uamuzi huo tarehe 12 Aprili 2015.[12] Tazama pia
Tanbihi
Tafsiri
Muziki uliorekodiwa
Marejeo
Viungo vya nje |