MwanamkeMwanamke ni mwanadamu wa jinsia ya kike, kwa maana anafaa kuwa mke. Ndiyo sababu kwa kawaida anaitwa hivyo aliyefikia utu uzima au walau amebalehe. Kabla ya hapo huwa anaitwa mtoto wa kike, binti, mwanamwali au msichana. Baada ya kuzaa anaitwa kwa kawaida mama, jina lenye heshima kubwa katika utamaduni wa aina nyingi. Akianza kupata wajukuu, anajulikana pia kama bibi. Wanawake ni takriban nusu ya binadamu wote, wengine huwa wanaume. Ndizo jinsia mbili ambazo zinahesabiwa kwa kawaida kati ya binadamu. Mwanamke ana tabia zake za pekee upande wa mwili, nafsi na roho, na tofauti kati yao na wanaume hujitokeza kwa namna mbalimbali katika utendaji. Katika maumbile ya mwili wanawake huwa na viungo vya uzazi vya kike ambavyo ni vya pekee na kulindwa kwa jumla ndani ya mwili. Msingi wa tofauti hizo ni hasa chembeuzi cha jinsia, yaani wanaume wana jozi la chembeuzi "X" na "Y" ndani ya seli zao zote, lakini wanawake wana jozi la "X" mbili. Chembeuzi Y inabeba habari zote zinazomfanya mwanadamu kukua kama mwanaume badala ya mwanamke. Lakini si tofauti za mwilini pekee zinazosababisha wanawake kuwa tofauti na wanaume. Kuna pia tabia za kiakili na za kiroho za pekee zinazoonekana wazi kati ya wanawake wengi. Hata hivyo tofauti nyingi zinategemea pia utamaduni kwa sababu mara nyingi watu wamepanga shughuli na pia namna ya maisha tofauti kwa wanaume na wanawake, hivyo watu wamezoea kuchukua matokeo ya mapatano hayo kama jambo la kimaumbile hata kama ni la kiutamaduni tu. Pamoja na hayo, kuna wanawake wenye tabia zinazotazamiwa kuwa za kiume. Sababu kuu ni kwamba miili yao huwa na viwango vya homoni tofauti na kawaida. Kuna watu kadhaa wenye mwili wa kike wanaojisikia kuwa wanaume, pengine kutokana na matukio ya utotoni au athari nyingine za kisaikolojia. Tazama piaMarejeo
Viungo vya nje
|