Zuhura
Zuhura ni sayari ya pili katika Mfumo wa Jua. Kati ya sayari zote za Jua ndiyo inayofanana zaidi na Dunia yetu. Asili ya jinaSayari hii ina majina mawili kwa Kiswahili: Zuhura, kwa matamshi mengine pia "Zuhra", ni jina leye asili ya Kiarabu زُهَرَة zuhara lenye maana asilia ya "mwenye kung'aa". Ng'andu ni jina lenye asili ya Kibantu. Tabia za sayariKwenye anga la usiku inang'aa kushinda nyota zote isipokuwa mwezi. Kutokana na nguvu ya mwanga wake inaonekana mapema kati ya nyota za kwanza zinazoonekana jioni; vilevile huwa inaonekana kama nyota ya mwisho wakati wa pambazuko. Zuhura ina umbali wa kati ya kilomita milioni 107.5 - 108.9 kutoka Jua. Umbali kutoka Dunia yetu hutegemea na mahali pa Dunia na Zuhura kwenye mizingo yao ya kuzunguka Jua: uko kati ya kilomita milioni 38.3-260.9. Ukubwa wake na pia kemia yake zinafanana sana na Dunia ikiwa kipenyo chake ni km 12,103.6 kwenye ikweta. Haina mwezi wowote. Mwaka wa Zuhura (ambao ni muda wa kutimiza njiamzingo moja wa kuzunguka Dunia) una siku 224.7 za Dunia. Siku ya Zuhura (ambayo ni muda wa duru moja ya sayari yenyewe) ina siku 243 za Dunia. Zuhura ni sayari yenye mzunguko kufuatana na mwendo wa saa. Hali ya hewa ni ya joto sana, kwa wastani sentigredi 500. Hewa yake ni hasa ya kabonidaioksaidi[1] inayosababisha mawingu mengi yanayozuia sura yake isionekane kwa darubini. Kutokana na halijoto kali hakuna maji. UtafitiWarusi na Wamarekani walifaulu kupeleka vipimaanga mbalimbali hadi Zuhura, vingine vilipita na kupima hewa, vingine vilifika kwenye sura ya sayari na kutuma picha za mazingira hadi kuharibika kutokana na joto kali. Uso wa sayari umefanyiwa utafiti kwa msaada wa rada kutoka vipimaanga Magellan na Pioneer-Venus. Kutokana na matokeo yake ramani ya kwanza ilitokea. Sehemu kubwa ya sayari ni tambarare yenye vilima na mabonde yasiyo marefu. Kutokana na joto kubwa (mnamo 500°C) hakuna maji wala bahari. Kuna sehemu mbili ambako nyanda za juu zinapanda juu ya uwiano wa kawaida na hizi zilifananishwa na kontinenti za Dunia. Karibu na ikweta ya Zuhura iko sehemu inayoitwa "Aphrodite Terra" yenye ukubwa kama Amerika Kusini. Kwenye upande wa mashariki kuna safu za milima na mabonde makubwa pamoja na volkeno. Sehemu ya pili huitwa "Ishtar Terra" yenye ukubwa sawa na Australia kwenye Dunia. Hapa kuna milima ya Maxwell yenye urefu wa mita 10.800 juu ya uwiano wa wastani. Marejeo
Viungo vya njeWikimedia Commons ina media kuhusu:
Kuhusu ramani za Zuhura
|