Mshtarii
Mshtarii ni sayari ya tano kutoka Jua katika Mfumo wa Jua, na sayari kubwa kabisa ya mfumo. Tungamo yake inazidi mara mbili na nusu masi ya sayari nyingine zote pamoja. AngahewaMshtarii haina uso unaoonekana. Sehemu kubwa ya tungamo ya sayari ni elementi nyepesi kama hidrojeni na heli ambazo ni gesi katika mazingira ya duniani. Hii ndiyo sababu ya kwamba sayari kubwa za Mshtarii pamoja na Zohali huitwa "sayari jitu za gesi". Kadiri gesi hizo zinavyopatikana chini zaidi (yaani kuelekea ndani) uzito wa matabaka ya juu unaongeza shinikizo katika vilindi vyake na kusababisha gesi za angahewa kuingia katika hali ya giligili (majimaji) inayobadilika kuwa mango ndani zaidi. Zamani iliaminika ya kwamba sayari yote ni ya gesi iliyoganda lakini siku hizi wataalamu wa anga huamini kwamba kuna kiini cha mwamba au metali. Doa jekundu linaloonekana usoni mwa angahewa ni dhoruba ya tufani kubwa sana iliyotazamwa tangu darubini za kwanza zilipopatikana. Duniani tufani zinapotea kwa kawaida baada ya wiki kadhaa lakini doa jekundu limeendelea bila kusimama kwa miaka 300. MieziMshtarii ina miezi 79 iliyotambuliwa hadi mwaka 2018[1]. Miezi minne mikubwa ilitambuliwa mwaka 1610 na Galileo Galilei aliyekuwa kati ya wanaastronomia wa kwanza kutumia darubini. Ndiyo Io, Europa, Ganimedi na Kalisto. Ukubwa wa Ganimedi unakaribia kipenyo cha Utaridi ukipita kile cha Pluto. Miezi 63 huwa na kipenyo chini ya kilomita 10. Mwezi mdogo kabisa wa Mshtarii unajulikana kwa namba tu na una kipenyo cha km 1. Marejeo
|