Iraq
Iraq (kwa Kiarabu العراق, al-ʿIrāq) ni nchi ya Asia ya Magharibi inayokaliwa hasa na Waarabu (75-80%) lakini pia na wengine, hasa Wakurdi 15%). Inajumlisha eneo la Mesopotamia pamoja na sehemu ya jangwa la Shamu na ya milima ya Zagros. Imepakana na Kuwait, Saudia, Yordani, Syria, Uturuki na Uajemi. Kuna pwani fupi kwenye Ghuba ya Uajemi. JiografiaSehemu kubwa ya Iraq ni jangwa lakini kuna eneo lenye rutuba kati ya mito ya Frati na Hidekeli. Kaskazini ni hasa nchi ya milima inayopanda hadi ya kimo cha m 3,611 juu ya UB. Hali ya hewa inalingana na mazingira. Kipindi cha kiangazi kuna joto kali. Majira ya Desemba-Februari kuna halijoto ya kupoa kusini na baridi kali mlimani. HistoriaIraq ni nchi yenye historia ndefuː ilikuwa kitovu cha ustaarabu wa binadamu, mahali pa miji ya kwanza duniani katika Sumeri na Babeli. Baada ya kusambaratika kwa milki ya Waturuki Waosmani walioitawala muda mrefu, Iraq ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Shirikisho la Mataifa mwaka 1932 ingawa hali halisi ilikuwa nchi lindwa chini ya athira ya Uingereza hadi mwaka 1958. Miaka ya hivi karibuni imejulikana hasa kutokana na vita mbalimbaliː kwanza vita dhidi ya Uajemi chini ya serikali ya Saddam Hussein tangu 1981, baadaye vita dhidi ya Kuwait na Marekani. Vita vya pili vya ghuba ya 2003 iliyoleta uvamizi wa Marekani ilizidi kuleta vifo na uharibifu. Hatimaye vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoingiliwa na DAESH iliyoteka sehemu kubwa ya nchi, hasa kaskazini na magharibi, hadi mwishoni mwa mwaka 2017. WatuLugha rasmi na ya kwanza ni Kiarabu, ikifuatwa na Kikurdi ambayo pia imekuwa lugha rasmi, halafu lugha nyingine za jamii mbalimbali ambazo pengine zinatambulika kieneo. Wakazi wengi (95%), hasa baada ya vita vya hivi karibuni, ni Waislamu, wakiwemo kwanza Washia halafu na Wasuni. Wakristo waliobaki ni 5%, wakiwemo hasa waamini wa Kanisa Katoliki la Wakaldayo na Waashuru wa Kanisa la Mashariki. UchumiIraq ina akiba kubwa za mafuta ya petroli ardhini. Mapato kutokana na mafuta yalileta maendeleo makubwa nchini hadi mwanzo wa kipindi cha vita vilivyoharibu sana nchi pamoja na uchumi wake. Tazama piaMarejeo
Viungo vya nje
|