John Magufuli
John Pombe Joseph Magufuli (alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 - 17 Machi 2021) alikuwa rais wa tano wa Tanzania, akitokea katika chama cha Mapinduzi CCM. Aliongoza kwa muda wa miaka mitano na nusu hadi kifo chake[1]. Aliwahi kuwa Mbunge wa jimbo la Biharamulo Mashariki katika bunge la kitaifa huko nchini Tanzania na tangu mwaka 2010 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.[2] Tarehe 12 Julai 2015 alichaguliwa kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi akiwa na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan. Tarehe 29 Oktoba 2015 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza kuwa rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wa kura 8,882,935 sawa na 58.46% pamoja na makamu wa rais Samia Suluhu Hassani. Tarehe 5 Novemba 2015 aliapishwa kama rais wa tano wa Tanzania, ingawa upinzani haukukubali matokeo hayo. Baada ya uchaguzi wa tarehe 28 Oktoba 2020 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilimtangaza tena mshindi pamoja na makamu wa rais Samia Suluhu Hassan kwa kura 12,516,252 sawa na 84.4% ingawa kulikuwa na malalamiko makubwa[3]. ElimuAlikuwa na Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Pia miaka 1991 – 1994 alisomea Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza na miaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati. Kabla ya hapo tena Magufuli alisomea diploma katika Chuo cha Mkwawa, Iringa, akichukua masomo ya Kemia na Hisabati, hiyo ilikuwa miaka 1981 – 1982. Upande wa sekondari, Magufuli alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa huko Iringa kipindi cha miaka 1979 – 1981. Kabla ya hapo miaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza na miaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera. Hapo kati alikwenda Jeshi la Kujenga Taifa huko Arusha kwa mujibu wa sheria. Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Uzoefu wa kaziMagufuli alipomaliza elimu yake ya ualimu katika chuo cha ualimu cha Mkwawa, mwaka 1982, alianza kutumia taaluma yake ya Kemia na Hisabati kwa kufundisha Shule ya Sekondari Sengerema hadi mwaka 1983. Baada ya hapo akafanya kazi kama Mkemia katika Chama cha Ushirika cha Nyanza huko Mwanza hadi mwaka 1995 kisha akaanza safari yake ya siasa kwa kugombea ubunge mwaka 1995 huko Biharamulo Mashariki, kazi ambayo anaifanya hadi tarehe 1 Agosti 2015. Akiwa Mbunge wa Biharamulo Mashariki huko Chato amekuwa Naibu Waziri na Waziri katika Wizara mbalimbali. Tangu mwaka 2000 hadi 2005 alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki. Mwisho 2010 – 2015: Waziri wa Ujenzi. Uchaguzi wa urais wa mwaka 2015Tarehe 22 Julai Magufuli alichaguliwa kukiwakilisha Chama cha Mapinduzi kama mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, 2015, alipongezwa na naibu katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro na balozi wa Marekani kwa Umoja wa Afrika Amina Salum Ali kwa kwenda kukiwakilisha chama.[5][6] Japokuwa alikutana na changamoto kubwa kutoka kwa mgombea wa chama cha upinzani Edward Lowassa katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, tume ya taifa ya uchaguzi ilimtangaza Magufuli ndiye mshindi kwa asilimia hamsini na nane. Mgombea mwenza, Samia Suluhu, pia alitangazwa kuwa makamu wa rais. Kuapishwa kwa Magufuli kulifanyika tarehe 5 Novemba 2015.[7] Ndani ya mwezi mmoja tangu alipoingia madarakani alianza kudhibiti matumizi mabaya ya fedha ndani ya serikali kwa kufuta baadhi ya sherehe zisizo na ulazima pamoja na kupambana kwa dhati na wakwepakodi. Hivyo alifanikiwa kujenga imani ya wananchi wengi wa Tanzania ambao kwa kiasi kikubwa walionyesha kuchoshwa na uongozi wa chama chake[8]. Tarehe 10 Desemba 2015 alitangaza baraza la mawaziri likiwa na watu 34 tu katika nafasi ya waziri au naibu waziri, ndiyo baraza lenye mawaziri wachache ukilinganisha na uongozi uliopita. Ufanyaji kaziRais John Magufuli alisifika kwa ufanyaji kazi hodari kama mtu asiyekubali umaskini unaosababishwa na watu, hasa kwa wafanyakazi wake. Ijapo matokeo ya kuchaguliwa kwake yalileta pingamizi kubwa, lakini kwanza alikuja kupendwa na watu wa taifa lake, hata mataifa mengine yalitokea kumpenda, kutokana na ufanyaji wa kazi na misimamo inayoleta maendeleo kama kuzuia sherehe za uhuru na kutaka siku hiyo watu wafanye usafi katika maeneo yao. Pia alikuwa mtu ambaye anapenda haki sawa kwa wote na huchukia rushwa, ambayo amefaulu kuipunguza kwa kiasi fulani, pamoja na kutambua na kuondoa wafanyakazi hewa na watumishi wasio na sifa. Hata hivyo wengine wengi, yakiwemo mataifa makubwa ya Ulaya na Amerika, walihoji jinsi alivyokabili matatizo ya Zanzibar kuhusu kurudia uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015 uliofutwa bila sababu ya kueleweka. Pia jinsi serikali ilivyozidi kufinya uhuru wa vyama vya upinzani kukutana na wananchi na uhuru wa vyombo vya habari kutoa taarifa muhimu[9]. Lawama hizo ziliigharimu Tanzania kunyimwa misaada ya Marekani na nchi nyingi za Ulaya. Lawama nyingine zilitokea nchini kwa jinsi alivyoshughulikia tetemeko la ardhi la mwaka 2016 kaskazini mwa nchi na uhaba wa mvua uliofanya wengi wazungumzie hali ya njaa, kitu ambacho mwenyewe hakukikubali. Wakati huohuo wengine walilalamikia uchelewaji wa kuajiri waliomaliza chuo pamoja na uchache wa pesa katika mzunguko. Baadaye alielekeza nguvu zake kupambana na madawa ya kulevya na ushoga. Hatua nyingine tena, iliyosifiwa na wengi, ni kupinga dhuluma ya kiuchumi kutoka kwa kampuni zilizochimba dhahabu kwa wingi na kusomba makontena ya makinikia zikiliingiza taifa hasara ya shilingi trilioni nyingi, zilizolinganalingana na bajeti ya serikali. Hatimaye serikali ilikubaliana na kampuni ya Barrick kufuta kampuni tanzu Acacia na kuanzisha mpya Twiga ambamo serikali inamiliki asilimia 16 za hisa. Mnamo Oktoba 2019 alifanikiwa kuhamia Dodoma, jiji lililoteuliwa tangu zamani kuwa makao makuu ya nchi. KifoKadiri ya taarifa rasmi, John Pombe Magufuli alifariki tarehe 17 Mei 2021 saa 12 jioni katika hospitali ya Mzena ya jijini Dar es Salaam[10]. Magufuli hakuonekana hadharani tangu tarehe 27 Februari 2021, kisha uvumi ulienea kuwa yeye ni mgonjwa.[11] Tarehe 10 Machi gazeti la Nation nchini Kenya lilitoa taarifa kwamba "kiongozi Mwafrika ambaye hakuonekana wiki mbili" amepokewa katika hospitali fulani mjini Nairobi akiwa na Covid-19. Wengi walihisi kiongozi asiyetajwa ni Magufuli[12]. Mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu alidai ameambiwa na watu ambao hakutaja kuwa Magufuli ndiye aliyetibiwa katika Hospitali ya Nairobi na kwamba kuna mipango ya kumhamisha Uhindi.[13] Lissu aliongeza baadaye kwamba Magufuli aliaga dunia mnamo tarehe 10 Machi.[14] Usiku wa tarehe 17 Machi 2021 Makamu wa Rais Samia Suluhu alitangaza kuwa Magufuli aliwahi kufariki Dunia mnamo saa 12 jioni kwenye hospitali ya Emilio Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa anatibiwa.[11][15][16] Hakueleza ugonjwa uliosababisha kifo lakini alisema marehemu aliwahi kuwa na matatizo ya moyo kwa miaka 10. Alitangaza kipindi cha siku 14 cha maombolezo ya kitaifa.[17] Mbali ya kutajwa kwa matatizo ya moyo ya marehemu, uvumi kuhusu Covid-19 kama sababu halisi ya kifo hicho uliendelea.[18][19] Mwili wa marehemu ulipelekwa Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam tarehe 20 Machi 2021. Idadi kubwa ya watazamaji ilisababisha msongamano ambamo watu 45 au zaidi walikufa baada ya kukanyagwa na wengine.[20] Magufuli alizikwa nyumbani kwao Chato, alikokuwa ameelekeza pesa nyingi za umma[21], tarehe 26 Machi 2021. Marejeo
|