Liturujia ya KilatiniLiturujia ya Kilatini ni aina ya liturujia ya Ukristo iliyoenea upande wa magharibi wa Dola la Roma ambapo ilitumika lugha ya Kilatini. Liturujia hiyo ilistawi Ulaya magharibi na Afrika kaskazini. Polepole liturujia ya Roma, mji mkuu wa Walatini uliotawala dola hilo, ilienea katika maeneo mengi ya Kanisa Katoliki, hasa kutokana na juhudi za makusudi za kaisari Karolo Mkuu za kuunganisha mataifa yaliyokuwa chini ya himaya yake. Baadaye Mtaguso wa Trento ulizidi kudai Wakatoliki wa magharibi wafuate wote liturujia ya Roma, isipokuwa kama liturujia yao maalumu yaliendelea zaidi ya miaka 200. Hivyo baadhi ya liturujia nyingine za Kilatini zimedumu mpaka leo, kama vile liturujia ya Ambrosi kandokando ya Milano (Italia), liturujia ya Kimozarabu hasa huko Toledo (Hispania), liturujia ya Braga huko Ureno na kidogo liturujia ya Lyon huko Ufaransa. Pia baadhi ya mashirika ya kitawa yanatunza liturujia za pekee.
|