Usultani wa ZanzibarUsultani wa Zanzibar ulikuwa nchi kwenye pwani ya Afrika mashariki kati ya 1856 na 1964. Tangu 1890 ilikuwa nchi lindwa chini ya Uingereza. Ilianzishwa wakati wa kugawa Usultani wa Omani mwaka 1856 ikaishia mwaka 1964 baada ya mapinduzi ya Zanzibar na muungano na Tanganyika uliozaa Tanzania. Sayyid Said kuhamia UngujaUsultani ulianzishwa wakati Sultani Sayyid Said alipoamua kuhamisha makao makuu yake kutoka Maskat (Omani) kwenda Unguja. Sayyid Said alikuwa Sultani wa Omani tangu mwaka 1804. Aliimarisha utawala wa Omani juu ya pwani ya Afrika ya Mashariki. Mwaka 1829 alifaulu kuteka Mombasa iliyokuwa mji pekee wa kujitegemea kati ya miji yote ya Uswahilini. Visiwa vya Unguja na Pemba vilikuwa chini ya Omani tangu mwaka 1689, Wareno walipofukuzwa katika pwani za Uswahilini. Biashara ya karafuu na watumwaSayyid Said aliona nafasi kubwa ya biashara ya karafuu kwa ajili ya soko la Uhindi na kwingineko. Mwaka 1829 akaanzisha mashamba ya mikarafuu kwa kutumia kazi ya watumwa kutoka bara. Biashara hiyo ikabadilisha uso wa mji wa Zanzibar wa karne ya 19 uliowahi kuwa kijiji kikubwa tu cha vibanda kando ya boma lililojengwa na Omani kama kizuizi dhidi ya Wareno. Baada ya azimio la mwaka 1832 la kuhamisha mji mkuu wa Omani kwenda Unguja, idadi ya wakazi wa mji ilikua haraka. Nchi za nje zikatambua mji mkuu mpya na kujenga uhusiano. Ubalozi wa Marekani ulijengwa mwaka 1837, Uingereza ukafuata mwaka 1841 na Ufaransa mwaka 1844. Sultani mwenyewe aliondoka kabisa Maskat mwaka 1840. Kukua kwa Zanzibar kulisababisha kukonda kwa mji wa Maskat Kugawiwa kwa Omani kulikuwa mwanzo wa ZanzibarBaada ya kifo cha Sayyid Sultan mwaka 1856, usultani wa Oman uligawiwa kati ya wanawe. Sayyid Majid bin Said Al-Busaid (1834/1835–1870) akawa Sultani wa kwanza wa Zanzibar na kaka yake Sayyid Thuwaini bin Said al-Said akawa Sultani wa Oman akitawala nchi hiyo bila maeneo ya Afrika ya Mashariki. Usultani mpya ulikuwa nchi yenye nguvu kati ya Rasi Delgado (mpakani na koloni la Kireno ya Msumbiji) hadi Mogadishu (Somalia). Athira yake ilienea kupitia njia za misafara ya pembe za ndovu na watumwa hadi mto Kongo. Wafanyabiashara kama Tippu Tip waliokuwa raia wa Usultani wakapita Tabora na Ujiji kwenda ziwa Tanganyika na kuingia ndani ya eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo. Wapagazi wao walibeba bidhaa kutoka Zanzibar zilizobadilishwa kwa pembe za ndovu hasa. Watumwa walikamatwa au kununuliwa wakabeba pembe hadi pwani. Pamoja na hayo, sultani alipokea kwa moyo wamisionari Wakristo. Mapadri Wakatoliki wa kwanza pamoja na masista walitokea Reunion wakakaa Unguja tangu tarehe 12 Desemba 1860 hadi mwaka 1863, walipokabidhi misheni kwa shirika la mapadri wa Roho Mtakatifu. Waanglikana wa chama cha Misheni ya Vyuo Vikuu kwa Afrika ya Kati U.M.C.A. (Universities` Mission to Central Africa) ambacho kiliundwa ili kutekeleza wito kutoka David Livingstone kuhubiri Injili na kukomesha utumwa katika Afrika, waliingia Zanzibar mwaka 1864. Baadaye wakajenga kanisa kuu mahali pa soko la watumwa lililofungwa, altari ikiwa imejengwa juu ya nafasi ya mti wa kuwafunga watumwa walioadhibiwa kwa viboko, na batizio kuwa mahali walipotupwa watoto watumwa ambao hawakuuzwa pamoja na mama zao. Sayyid BarghashSultani wa pili wa Zanzibar yenyewe, Sayyid Barghash (1870-1888), alijitahidi kujenga uhusiano na nchi za nje. Alifunga soko la watumwa Zanzibar mjini kulingana na mapatano ya kimataifa, lakini akavumilia biashara ya watumwa kuendelea chinichini. Wakati wa Barghash majengo mengi ya Mji Mkongwe yakajengwa. Barghash alikuwa na wanajeshi wa kudumu. Mwanzoni alitumia mamluki walioajiriwa kutoka Uarabuni na Uajemi, hasa Baluchistan, pamoja na watumwa[1]. Kuanzia mwaka 1877 alianzisha kikosi kipya cha askari mia kadhaa chini ya afisa Mwingereza Lloyd Mathews waliofundishwa kufuatana na utaratibu wa Kizungu; askari hao waliteuliwa chini ya Waafrika wa Unguja.[2] Mwishowe mwa utawala wake aliona kupungukiwa kwa eneo lake kutokana na mashindano ya nchi za Ulaya ya kuenea katika Afrika baada ya mkutano wa Berlin wa 1885. Mwaka 1885 Karl Peters alifanya mikataba ya ulinzi na watawala wadogo waliokuwa chini ya Sultani barani Tanganyika. Upingamizi wa Sultani ulishindikana kwa sababu Wajerumani walituma manowari Unguja akapaswa kukubali maeneo mapya ya Wajerumani. Kuenea kwa ukoloniMwaka 1886 mkataba kati ya Uingereza na Ujerumani ulibana eneo la sultani barani katika kanda yenye upana wa maili kumi tu kati ya Rasi Delgado na Mogadishu. Barghash na mfuasi wake Khalifa bin Said waliamua kuuza maeneo hayo au kuyakodisha.
Hali halisi usultani ukabaki na visiwa viwili vya Unguja na Pemba tu. Waingereza walikuwa walisita kuhusu Zanzibar lakini baada ya jaribio la Karl Peters la kufanya mkataba na Sultani ili kuingiza visiwa hivyo katika Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, Uingereza uliamua kutafuta utawala wa visiwa. Mkataba wa Zanzibar-Heligoland na mwisho wa uhuruMkataba wa Zanzibar-Helgoland kati ya Ujerumani na Uingereza ulileta patano la kuwa Zanzibar itakuwa chini ya Uingereza. Tangu mwaka 1890 waziri mkuu wa Sultani alikuwa Mwingereza aliyepokea amri kutoka London. Tangu mwaka 1913 nafasi ilichukuliwa na afisa mkazi mkuu. Kwa muda wa miaka 26 usultani ulikuwa na fedha yake ya pekee iliyoitwa Riali ya Zanzibar. Uhuru 1963 na mapinduziZanzibar ilipata uhuru wake tarehe 10 Desemba 1963. Uhuru wa usultani ukadumu muda mdogo tu. Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964 yakamuondoa Sultani. Mauaji ya familia nyingi zenye asili ya Kiarabu yakafuata. Tarehe 26 Aprili 1964 Zanzibar ikaunganika na Tanganyika kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Masultani wa Zanzibar
Mawaziri
Maafisa wakazi wakuu
Tanbihi
Information related to Usultani wa Zanzibar |